Robo yake yatosha kugharimia matangazo �laivu� ya Bunge TBC kwa miaka minne
Wakati serikali ikitangaza kupunguza muda wa kurusha matangazo ya moja kwa moja kupitia kituo cha televisheni cha Shirika la Habari la Taifa (TBC) kutokana na gharama kubwa za kufanikisha jambo hilo zinazofikia Sh. bilioni 4.2 kwa mwaka, imefahamika kuwa walau robo tu ya jumla ya posho wanazolipwa sasa wabunge kinaweza kutatua tatizo hilo na kuwapa wananchi haki ya kufuatilia kila nuktaya michango ya wawakilishi wao ndani ya chombo hicho kwa mwaka mzima.Uchunguzi uliofanywa na Nipashe umebaini Serikali italazimika kutumia Sh. bilioni 14.15 kwa ajili ya kuwalipa posho wabunge katika siku za vikao zinazokadiriwa kuwa 120 kwa mwaka, sawa na Sh. bilioni 70.75 kwa miaka mitano ya kipindi chote cha ngwe ya kwanza ya uhai wa Bunge la 11.Kiwango hicho (Sh. bilioni 14.15) ni zaidi ya mara tatu ya gharama za kurusha matangazo ya moja kwamoja ya vikao vya Bunge kwa mwaka zilizotajwa bungeni na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye.Jumatano wiki hii, Nnauye alizua sokomoko bungeni kutokana na tangazo alilotoa kuwa kuanzia sasa, TBC haitarusha tena ‘laivu’ matangazo yote ya Bunge bali sehemu tu ya kipindi cha maswali na majibu nyakati za asubuhi na kisha usiku kuonyesha marudio ya mijadala mbalimbali kwa muda wa saa moja, katika maeneo yenye "umuhimu kwa taifa".Nape alidai uamuzi huo umefikiwa ili kuepuka gharama kubwa kwa TBC za urushaji wa moja kwa moja wa matangazo hayo.Novemba 24 mwaka jana, Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu, aliiambia Nipashekuwa posho wanazolipwa wabunge hivi sasa ni Sh. 300,000, mchanganuo wake ukiwa ni Sh. 80,000 za kujikimu maarufu kama ‘per diem’ huku kiasi kingine cha Sh. 220,000 kikitolewa wanaposhiriki vikao, maarufu kama ‘sitting allowance’.Aidha, Kingu aliyekuwa akizungumza na Nipashe kuelezea uamuzi wake wa kutochukua ‘sitting allowance’ na kuliandikia Bunge akitaka posho hiyo ielekezwe jimboni kwake kwa ajili ya kusaidia shughuli za maendeleo, alisema kwa wastani, vikao vyote vya Bunge kwa mwaka mmoja huchukua siku 182. Hata hivyo, Nipashe haikuweza kuthibitisha idadi ya siku za vikao vya Bunge kwa mwaka kwani hesabu nyingine zinaonyesha kuwa hazizidi 120, ambazo ni wastani wa wiki mbili za za vikao vya Bunge la Januari, miezi mitatu Bunge la Bajeti na wiki nyingine mbili za Bunge la Novemba.Hivi sasa, kwa mujibu wa ibara ya 66 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, idadi ya wabunge wote wakitimia ni 393.Idadi hiyo ni wabunge 264 wa kuchaguliwa kutoka kwenye majimbo nchini, viti maalum 113, wabunge watano kutoka Baraza la Wawakilishi, wabunge 10 wa kuteuliwa na Rais na pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali anayeingia kutokana na nafasi yake.Hata hivyo, hadi kufikia jana, tovuti rasmi ya Bunge (www.parliament.go.tz) ilikuwa ikionyesha kuwa wabunge waliopo ni 382.Kwa sababu hiyo, endapo wabunge wote 393 watakuwapo bungeni na kila mmoja kulipwa posho ya Sh. 300,000 katika siku walau 120 za vikao vya Bunge kwa mwaka, maana yake jumla ya fedha zitakazolipwa na Serikali kugharimia vikao vya chombo hicho kwa mwaka ni Sh. bilioni 14.15, na Sh.bilioni 70.74 kwa miaka yote mitano ya uhai wa Bunge la 11, hasa ikiwa kiwango hicho hakitabadilika.Aidha, kama ‘sitting allowances’ (Sh. 220,000) zinazopingwa na baadhi ya wabunge wakiwamo Kingu na Zitto Kabwe wa Jimbo la Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) zitapunguzwa walau kwa kiwangocha nusu yake tu kwa kila mbunge (Sh. 110,000), maana yake zitapatikana jumla ya Sh. bilioni 5.12 kwa mwaka ambazo zitatosha kugharimia matangazo yote ya moja kwa moja ya Bunge kupitia TBC kwa kipindi hicho ikiwa kiwango cha posho na gharama za matangazo (TBC) havitabadilika.Baada ya tangazo la Nape kuhusiana na kusitishwa kwa baadhi ya matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kupitia TBC, mabishano makali yalitokea kutokana na wabunge wa kambi ya upinzani kupingahatua hiyo kwa maelezo kwamba wananchi wana haki ya kuona namna wabunge wao wanavyowawakilisha bungeni na kuituhumu serikali kuwa imechukua uamuzi huo kwa nia ya kuficha aibu baada ya ‘madudu’ mbalimbali yaliyowahi kuibuliwa na wawakilishi hao, na kuilazimu serikali kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri mara tano katika Bunge la 10 lilopita.Baadhi ya kashfa kubwa zilizowahi kuibuliwa bungeni na kushuhudiwa moja kwa moja na wananchi kupitia TBC ni Richmond iliyosababisha kuvunjwa kwa baraza zima la mawaziri mwaka 2008, Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), Operesheni Tokomeza iliyowang’oa mawaziri wanne na Akaunti ya Tegeta Escrow iliyowaondoa mawaziri wawili.Kadhalika, wapo wananchi walioishutumu serikali kwa kudai kuwa inawanyima wananchi haki yao ya kuona kila kinachotendwa na wawakilishi wao bungeni kwa kisingizio cha gharama.Wananchi hao walisema lengo la TBC siyo kufanya biashara na uendeshaji wake hutegemea kodi za wananchi.Baada ya tangazo la Nnauye, vurugu kubwa ziliibukana polisi zaidi ya 50 waliripotiwa kuingia bungeni na kutembeza kipigo kwa baadhi ya wabunge kufuatia agizo la Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, aliyetka kuondolewa kwa wabunge wa upinzani waliokuwa wakipinga hatua hiyo ya serikali.Juzi, wabunge wa upinzani walitoka nje ya ukumbi wa Bunge kupinga msimamo wa serikali wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya TBC.Akizungumzia kusitishwa kwa badhi ya matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kupitia TBC, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicholaus Mgaya, alipinga hatua hiyo ya serikali akisema tangazo hilo la Waziri ni sawa na kuwanyima haki wananchi.Aliitaka serikali kubana matumizi katika maeneo mengine, ikiwamo hata kushauriana na wabunge ili kupunguza posho za vikao (sitting allowances) kutoka Sh. 220,000 wanazopata sasa hadi kufikia Sh.50,000 ili kuwezesha matangazo ya Bunge kuendeleekurushwa moja kwa moja kupitia TBC ambayo lengo lake kuu halipaswi kuwa kuzalisha faida bali kutoa huduma kwa umma.“Vikao vya bunge ni sehemu ya kazi za wabunge ambalo ni jukumu lao… lakini pia serikali inapaswa kuendelea kubana matumizi katika maeneo mengine na kuacha posho za wabunge itakuwa haijafanya kitu. Ni vyema posho zikapunguzwa ili kufidia mambo mengine ikiwamo kurusha matangazo ya bunge moja kwa moja,” alisema Mgaya.Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Salum Mwalimu, aliwaambia waandishi wa habari kuwa chama chake kipo tayari kuchangisha fedha za kugharimia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge, huku akitilia shaka gharama zilizotajwa na Nape kuwa ni za juu kuliko uhalisia.HAKI ZA BINADAMU WATOA KAULIKituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa taarifa ya kupinga hatua ya serikali kusitishabaadhi ya matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja kupitia TBC kwa madai kwamba inaepuka gharama.Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Emelda Urio, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa hatua hiyo ya serikali inakwenda kinyume cha sheria na haki ya wananchi ya kupata taarifa na uhuru wa kutoa maoni.“Haki hizi ni muhimu katika kukua kwa demokrasia na misingi ya utawala bora. Ibara ya 21 (2) ya Katibaya Tanzania inaeleza kuwa, kila raia ana haki na uhuru wa kushiriki kwa kikamilifu katika uamuzi juu ya mambo yanayomuhusu yeye, maisha yake au yanayolihusu taifa lake na pia kupata taarifa,” alisema Urio.Aliitaka serikali kuheshimu haki ya kupata taarifa nauhuru wa habari kwa kuweka mazingira wezeshi kwaWatanzania wote kupata habari na taarifa zinazowahusu kwa wakati ambazo ni wezeshi kuwafanya wachukue maamuzi sahihi.Pia aliitaka serikali kutekeleza kwa vitendo maazimiona makubaliano ya kimatafa ya kikanda katika kulinda haki ya kupata taarifa kwa kufuata sheria kandamizi zenye kuminya uhuru.Urio alisema serikali inatakiwa iache kuminya haki za Watanzania kwa kisingizio cha gharama na badala yake itenge rasilimali za kutosha kuwezesha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kwa TBC.Mtaalamu wa masuala ya siasa, Paul Mandawa, alisema kwa mtazamo wake, posho wanazolipwa wabunge ni kubwa na kwamba zingeweza kupunguzwa ili kusaidia shughuli za maendeleo ya kijamii kama upatikanaji wa maji safi, ujenzi wa shule na ununuzi wa dawa hospitalini.Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Namibia, Idara ya Uandishi wa Habari, Julius Mtemahanji, alisema wakati umefika kwa wabunge kutumia busara katika kutimiza wajibu wao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni