Nianze kwa kuwapa salamu Watanzania wenzangu mliojaa uzalendo, mlio tayari kuhoji mambo ya msingi kwa mustakabali wa nchi yetu.
Nawapongeza kwa sababu mnajitambua na angalau
mnaweza kuwatia kashikashi viongozi wa Serikali pale ambapo wanasahau
majukumu yao.
Nia yangu si kuponda tabia za baadhi ya Watanzania
wenzagu ‘waliolala’, lengo langu ni kuwapa ushauri tu kwamba hata kama
wanashabikia mambo yasiyo na faida katika maisha yao, wakumbuke kuwa
kuna mambo ya muhimu yanahitaji kupigiwa kelele kama si kupingwa.
Wananchi ndio wenye nchi, hivyo wanapaswa
kuhakikisha kuwa nchi yao ipo katika njia sahihi. Hata nchi
zilizoendelea zilifikia hatua hiyo baada ya wananchi wake kujitambua.
Hapa kwetu Tanzania baadhi ya wananchi wamekuwa mahodari kuhoji na hata kufuatilia, mambo ambayo hayawezi kuwasaidia hata kupata mlo wa usiku tu.
Kila mtu analikumbuka lile sakata la Miss Tanzania
2014, Sitti Mtemvu. Mwanadada huyu aliyetwaa taji la urembo,
anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kudanganya umri
wake, kitu ambacho ni kinyume na kanuni za mashindano hayo ya urembo.
Sakata hilo lilikuwa mjadala katika mitandao ya kijamii, vijiweni, katika daladala na hata kwenye baadhi ya maofisi.
Ni kweli kabisa mrembo huyo wa Tanzania anakwenda kuiwakilisha
nchi, lakini tujiulize nguvu iliyotumika kumpinga Sitti ina faida gani
kwa wananchi maskini.
Umejaribu kufikiri Miss Tanzania inasaidiaje
kuboresha maisha yako na wananchi wengine walioko vijijini. Miss
Tanzania inaweza kuleta huduma bora za afya?
Vipi kuhusu elimu, unadhani Miss Tanzania inaweza kuisaidia nchi kujenga mabweni, maabara, kununua madawati. Jibu ni hapana.
Mambo niliyoyataja hapo juu ni baadhi tu
yanayotakiwa kupigiwa kelele na idadi kubwa ya Watanzania ili kuifanya
nchi yetu iweze kupiga hatua kama nchi nyingine ambazo miaka 1960
zilikuwa hazina tofauti ya kiuchumi na Tanzania.
Sikatai watu kumpinga, kinachonishangaza ni tabia ya walio wengi ya ‘kushupalia’ jambo hili au mengine yanayofanana na hilo huku wakiacha kujadili mengine ya msingi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni