Dar es Salaam. Mwanamuziki wa kike, Vanessa Mdee maarufu kwa jina la Vee Money, amewataka wasanii kujituma katika kazi na kuachana na fikra hasi anazoamini ni kikwazo kwa walio wengi.
Vee Money, aliyeonekana kwenye shoo ya Kourtney
And Khloe Take The Hamptons (The Kardashians) inayoonyeshwa na kituo cha
E! Entertainment cha Marekani, wikiendi iliyopita aliliambia gazeti
hili kuwa wengi huathirika kisaikolojia kutokana na mawazo hasi
wanayokuwa nayo hasa wanapokutana na changamoto ambazo ni za kawaida
katika utafutaji.
“Walio wengi hupata fikra hasi hasa wanapokumbana
na changamoto. Ijulikane kwamba hakuna anayefanya kazi bila kupata
vikwazo, hakuna kazi nyepesi. Sasa wakikumbana nazo wanaamini kwamba
kuna fitina za mtu au watu,” alisema msanii huyo anayetamba na wimbo
wake wa “Hamjui”. Akielezea mtazamo wake katika hilo, Vee Money alisema
haamini kama kuna fitina katika muziki na katu hawezi kupoteza muda
kufikiria mambo kama hayo.
“Sina imani hizo na hata kama ikija kunitokea
sitaamini bali nitajua ni sehemu ya changamoto za kikazi au maisha kisha
nitasonga mbele. Unajua tunapoteza muda kwa kuwa na imani potofu, hata
kama fitna zitakuwepo onyesha uwezo wako usikubali zikupoteze,” alisema.
Alisema wasanii wengi hupotea kutokana na kuamini nguvu ya fitna na mwisho wa siku wanashuka kimuziki. “Wengi wanashuka kimuziki kwa kukosa plan B,
japokuwa wengine hulewa sifa na kutokuwa na usimamizi mzuri ni moja ya
sababu pia,” alisema Vee Money.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni