​WAZIRI MKUU WA TANZANIA MH KASSIM MAJALIWA APOKEA SH. MILIONI 5.6 ZA MADAWATI - MKWELI BLOG

Karibu kwenye kitovu cha HABARI.

PATA HABARI ZA MICHEZO KUTOKA KILA KONA YA DUNIA NA MAGAZETI KWA WAKATI UKIWA KARIBU NASI

Breaking

Home Top Ad

Responsive Ads Here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Jumatano, 15 Februari 2017

​WAZIRI MKUU WA TANZANIA MH KASSIM MAJALIWA APOKEA SH. MILIONI 5.6 ZA MADAWATI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma nchini wawe wabunifu katika kusaidia kutafuta vyanzo vya mapato kwenye jamii inayowazunguka.

Ametoa wito huo leo (Jumanne, Februari 14, 2017) ofisini kwake mjini Dodoma mara baada ya kupokea mchango wa sh. milioni 5.6 kwa ajili ya kununulia madawati 70 kutoka kwa watumishi wa TAMISEMI – Dodoma.

Amesema ubunifu huo uliofanywa na watumishi wa TAMISEMI, ni mfano mzuri wa kuigwa na watumishi wengine nchini kwani utaisaidia Serikali kuleta maendeleo.

“Hii ni mara ya tatu kwa TAMISEMI kuchangia huduma za jamii kwenye maeneo mbalimbali nchini… lakini pia niwashukuru kwa kuchagua jimbo la Ruangwa kuwa miongoni  mwa maeneo ambayo ni wanufaika wa mchango wenu,” amesema.

“Mchango huu ni mkubwa na utasaidia mikondo miwili kwa shule za sekondari. Tunahitaji kupata mawazo mapya kama haya, na tunahitaji wafanyakazi wengine wajifunze kutoka TAMISEMI,” amesema.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi mchango wao, kiongozi wa ujumbe ulioenda kuwasilisha mchango kwa Waziri Mkuu, Bw. Filbert Rwakilomba amesema lengo lao ni kuchangia madawati 100 lakini wameamua kutanguliza mchango wa madawati 70 na baada ya siku mbili watakabidhi mchango wa madawati 30 yaliyobakia.

Bw. Rwakilomba ambaye anaongoza kamati ya watu 30 ambao ni watumishi kutoka idara tofauti za Ofisi ya Rais TAMISEMI Dodoma, amesema wametoa mchango huo kama ishara ya kuenzi kazi aliyoifanya Waziri Mkuu Majaliwa wakati akiwa Naibu Waziri (TAMISEMI – Elimu).

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

    L. P. 980,

DODOMA.

JUMANNE, FEBRUARI 14, 2017.


Hakuna maoni:

Post Bottom Ad

Responsive Ads Here

Kurasa