Baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kutangaza matokeo ya kidato cha nne na kuonyesha kiwango cha ufaulu kimeshuka kwa asilimia 1.85 ukilinganisha na mwaka jana, taasisi na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu wameishushia lawamaserikali kwa kutowajali walimu huku ikiajiri baadhi wasio na sifa.Katika matokeo hayo ya kidato cha nne 2015 yaliyotangazwa jana, yanaonyesha wanafunzi waliofaulu daraja la kwanza hadi la tatu ni asilimia 25 huku waliopata daraja la nne na sifuri, wakiwa asilimia 74.66.
RAIS CWT
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, amesema kushuka kwa kiwango cha ufaulu, kwake siyo kigezo pekee cha kuboresha elimu, bali serikali inapaswa kujipanga kurudisha hadhi katika sekta hiyo kama enzi ya mkoloni."Lazima serikali kuwa makini katika utoaji wa ajira za walimu na kuwaboreshea maslahi yao ili wafanye kazi kwa moyo badala ya kuendelea kunung’unikia maisha magumu," alisema Mukoba.Alisema haiwezekani mwanafunzi afanye vizuri katika mitihani wakati amekaa juu ya jiwe na kwamba tofauti lazima itajionyesha kati yake na mtoto anayesoma katika mazingira mazuri.“Serikali ikiboresha mfumo wa upatikanaji wa walimu bora na maslahi yao, elimu itapanda kama ilivyokuwa wakati wa mkoloni. Tutapoteza muda kujadili matokeo kila yanapotoka, tunapaswa kuangalia mzizi wa tatizo ili tuung’oe,” alisema na kuongeza:"Mwanafunzi anayepata alama A na yule anayepata D, ukizungumza nao, aliyepata alama D, huoyesha uwezo mkubwa kuliko aliyepata alama A. Hii ni tofauti kubwa iliyopo katika suala la utoaji elimu."Alisema kipaumbele chake siyo madaraja ya ufaulu, suala la msingi ni kuwaandaa wanafunzi kufaulu mitihani na maisha yao ya baadaye baada ya kuhitimu.
HAKI ELIMU
Meneja wa Idara ya Utafiti na Sera wa Haki Elimu, Bonaventure Godfrey, alisema serikali inapaswa kuboresha mazingira ya kufundishia na kuweka mfumo bora wa ukaguzi kwa walimu ili kubaini wanafundisha au la.Alisema wanafunzi wa shule binafsi wanafanya vizuri kutokana na mazingira yao mazuri ya kufundishia, ubora wa vifaa vikiwamo vitabu na maabara.“Kiwango cha ufaulu kinaonyesha kushuka kidogo ukilinganisha na mwaka jana, lakini kinatoa tafsiri mbaya ya ufaulu kuwa kati ya watoto 100 waliofanyamtihani, ni wanafunzi 25 wenye uwezo wa kujiunga na kidato cha tano, hii ni hali mbaya,” alisema.Godfrey alisema serikali inatakiwa kutoruhusu matabaka ya utoaji wa elimu katika ya shule binafsi ambazo kwa asilimia 90 zinafanya vizuri kuliko shuleza umma.
TWAWEZA
Shirika lilisilo la kiserikali la Twaweza kwa kushirikiana na Uwezo ambalo limekuwa likifanya tafiti mbalimbali ikiwamo upande wa elimu kwa ujumla, kwa upande wake limesema kushuka kwa kiwango cha ufaulu ni matokeo ya maandalizi mabaya wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi na kujiunga na sekondari.Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Uwezo, Zaida Mgalla, baada ya Piwax kutaka maoni juu yamatokeo ya kidato cha nne kushuka kiwango cha ufaulu ukilinganisha na mwaka jana.Alisema utafiti uliofanywa na Uwezo mwaka jana ulionyesha asilimia 20 ya wanafunzi wa darasa la saba walikuwa hawajui kusoma na kuandika na asilimia 30 hawajui kusoma Kiingereza.“Kama mtoto anamaliza shule hajui kusoma wala kuandika, wengine wanaojitahidi kidogo ndiyo wanachaguliwa kujaza nafasi katika shule za sekondari za kata, hayo leo ndiyo matokeo,” alisema.Mgalla alisema serikali inapaswa kuangaliwa vizuri uwajibikaji wa walimu, huku wakiendelea kuboresha maslahi yao ili wasikate tamaa, jambo litakalopunguza idadi ya wanafunzi 113,000 waliopata alama sifuri kurudi kijijini.
TAMONGSCO
Piwax ilipomtafuta Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (Tamongsco), Benjamin Nkonya, kwa njia ya simu alipokea na kusema hana hakika kama kiwango cha ufaulu kimeshuka au kimepanda.
PROF. KITILA
Kwa upande wa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Kitila Mkumbo, alisema tatizo linachochangia kushuka kwa kiwango cha elimu nchini ni kutokana na kutokuwa na uwekezaji mzuri katika sekta ya elimu.Alisema Tanzania itakuwa vigumu mno sekta ya elimu kusonga mbele endapo mazingira ya sekta hiyo hayataboreshwa ipasavyo.Prof. Kitila alisema mpaka sasa hakuna walimu wa kutosha hasa katika masomo ya hisabati, vifaa, lakini pia mazingira yenyewe ya walimu hao ya kuwawezesha kupenda kazi yao hayajaboreshwa.Aliongeza kuwa kuboreshwa kwa sekta ya elimu kwaTanzania itachukua kati ya miaka 10 hadi 15 ijayo kwa sababu badala ya kuboresha mazingira ya elimu, serikali imekuwa ikipigania zaidi katika kuongeza idadi ya wanafunzi.Alisema imefika wakati sasa kwa Serikali ya awamu ya tano kuchukulia suala hilo kama changamoto kwake kwa kuhakikisha inafanyia kazi upungufu wote uliopo katika sekta hiyo ikiwamo kuhakikisha inaajiri walimu wa kutosha na wenye sifa na uwezo wa kufanya kazi.Kadhalika, alisema inapaswa ielekeze nguvu zake katika kuongeza idadi sahihi ya walimu wenye uwezo katika sekta hiyo, kuboresha mazingira ya walimu pamoja na kuhakikisha vifaa vinakuwapo.
MWENYEKITI TAPIE
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji Binafsi katika Elimu (Tapie), Mohamed Mringo, alisema kushuka kwa kiwango cha ufaulu nchini kunachangiwa na kuajiriwa kwa walimu wachache wenye sifa hasa katika masomo mbalimbali hususan Sayansi, Hisabati na Kiingereza.“Kuboreka kwa elimu nchini kutachukua muda mrefukwa sababu bado mizizi mizuri katika sekta hiyo haijawekwa, wanafunzi hawawezi kufaulu kama walimu wazuri wa kuwafundisha hawapo, hata wakipatikana wachache hasa katika masomo ya hesabu na sayansi, nao wanakuwa hawana uwezo wa kutosha,” alisema na kuongeza:“Kwa upande wa masomo ya sayansi, wapo wanafunzi wanaopenda kusoma masomo hayo, lakini wanakosa walimu wazuri wa kuwafundisha, vifaa vya kuwasaidia kufaulu masomo hayo navyo hakuna, sasa hapo utegemee matokeo gani?.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni