Mbunge wa Geita,Donald Max
1. Mtason Mtagwamba, mkazi wa Kijiji cha Nyantorotoro
Uliwaahidi wakazi wa Kijiji cha Nyantorotoro,
Geita maji baada ya kuwaona wanateseka kwa kunywa maji ya chumvi na
meupe kama maziwa, lakini mpaka leo bado wanateseka.
Jibu: Tulikuwa tumekubaliana na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kusaidiana kuleta maji Geita.
GGM ilikamilisha sehemu yake ambayo ni ya kuvuta
maji kutoka Ziwa Victoria lakini Serikali ikawa imekwama kusambaza maji
kwa wananchi kama tulivyokuwa tumekubaliana.
Lakini tulikaa tukakubaliana na GGM ikamilishe
programu hiyo ya kusambaza maji kwa wananchi na mpaka sasa taratibu ziko
hatua ya mwisho hivyo wananchi wote wa Geita watapata maji kabla mwaka
huu wa 2014 haujaisha.
2. Paulo Vicent.
Wananchi wa Geita wamebarikiwa kwa kuwa na madini
lakini wanaishi kama wakimbizi, wananyan’ganywa ardhi wanapigwa virungu
na kuitwa wezi. Ulituahidi kutatua tatizo la wachimbaji wadogo lakini
mpaka leo wachimbaji wanakufa kwa kupigwa virungu wanapokwenda kuchimba
kwenye maeneo ya wawekezaji na hata maeneo yao wanayochimba ikigundulika
kuna dhahabu wanafukuzwa na kuambiwa eneo la mwekezaji utatueleza nini
juu ya hili?
Jibu: Naomba niseme kuwa mbunge hajawadharau
wachimbaji wadogo na suala la maeneo ya kuchimba wachimbaji wadogo
linaendelea kushughulikiwa.
Lakini mpaka sasa kuna viwanja 18 vimetengwa kwa
ajili yao maeneo ya Isamilo na Rwenge. Lakini suala la wachimbaji wa
samina na Mpovu hilo eneo ni la mwekezaji na wachimbaji wadogo
wanatakiwa kuondoka.
3 Wales Steaven, mkazi wa Kalangalala
Wakati unagombea ulituhahidi maji wakazi wa
Kalangalala na Nyankumbu ndani ya miezi mitatu, ukasema kwa kinywa chako
kama usipotekeleza ahadi hiyo kwa muda huo tukikuona tukukate kichwa.
lakini ulivyotuacha ndivyo tulivyo hadi leo. Kwa nini uligombea wakati ulijua huwezi kutekeleza ahadi?
Jibu: Kama nilivyokwishaeleza hapo awali kwamba maji yanakuja na mbunge licha ya kuwa anaumwa kwa kweli anajitahidi.
Ninachoweza kusema hapa ni kwamba hatujapata fedha kutoka Serikali kuu ambayo ni bajeti ya halmashauri.
Baadhi ya ahadi za mbunge zimechelewa kukamilika
kwa wakati kutokana na ufinyu huo wa bajeti. Lakini tumeiomba GGM
itusaidie kusambaza maji katika mji wa Geita.
Maji yanakuja wameshaanza kuchimba mitaro hivyo
kabla ya uchaguzi maji yatakuwa yamefika, wananchi wawe na subira, wawe
na imani na mbunge wao najua ahadi zote zitatekelezwa kwa asilimia 80
kabla uchaguzi.
4. Zawadi John, mkazi wa Nyakumbu
Wananchi wa kijiji cha Nyakumbu tuna tatizo la
maji, kina mama tunatembea umbali mrefu na kupigania maji kwenye visima
vya asili. Tunakunywa maji yenye mekyuri, ngozi zetu zinakakamaa kwa
kuoga maji machafu. Ulituhahidi Nyankumbu itabubujika maji lakini hadi
leo tunaelekea uchaguzi hakuna kitu unatueleza nini?
Jibu: Suala la maji nimeshalizungumza, nimesema
yanakuja kabla ya mwaka huu kuisha. Niseme Mbunge hajawaahidi uongo,
ahadi zake zote zinashughulikiwa na zitatekelezwa kama ilivyopangwa.
5. Jotham Mabula, mkazi wa Karangara
Nakumbuka wakati unaomba kura zetu katika Viwanja
vya Nyankumbu na Karangara ukiwa amepiga Magoti uliahidi maji lakini
mpaka leo tuko hivyohivyo. Kipi umetufanyia wananchi katika ahadi zote
ulizotoa?
Jibu: Suala la maji nimeshalijibu, ninachoweza kusema hapa ni juu ya mambo aliyoyafanya mbunge.
Kabla hajaugua amefanya yafuatayo. Ameezeka kituo cha Polisi Nkome, ametoa mabati na kuezeka kituo cha Polisi Kakubilo.
Pia amejenga shule mbili kwa kata 19, pia
amepeleka fedha za kutengeneza madawati kwa kila kata za Jimbo la Geita
zaidi ya Sh69 milioni.
Wanafunzi wa shule hizo wanakaa vizuri kwenye madawati, pia
amepeleka mabati 120 kwa kata 19 ya kuezeka shule za msingi na
sekondari.
6. Erick Tarimo, mkazi wa Geita
Geita tuna tatizo la barabara, alituahidi wananchi
wa Msalala Road kuwa tutakuwa na barabara baada ya kuoana ni mbovu na
hatuna sehemu ya kupitisha magari ya kubeba wagonjwa, lakini mpaka leo
hazijatengenezwa,kwa nini?
Jibu: Mpaka sasa barabara zinajengwa katika maeneo mbalimbali ya mji wa Geita ikiwamo Msalala Road.
Tumejenga barabara ya hapa mjini kwa kiwango cha
lami na tunaendelea na ujenzi wa barabara za mkoa ikiwamo ya kutoka
Geita kwenda Kasota na Nkome.
7. Baraka Enock, mkazi wa Geita
Nataka kujua kutoka kwako, wachimbaji wadogo wa
Samina wametengewa maeneo gani? Wakati unagombea ulisema kila mchimbaji
wa Geita atakuwa na eneo la kuchimba na hakuna wa kuwanyanyasa. Lakini
leo wachimbaji wanateseka.
Jibu: Wachimbaji wadogo wametengewa maeneo ya Isamilo na Rwenge na bado tunaendelea kutafuta maeneo mengine.
Mbunge hajawasahau wachimbaji wadogo, anawakumbuka
sana na ndiyo maana anahangaika kutafuta maeneo mengine kwa kuwatumia
madiwani.
8. Elizabeth Msusa, mkazi wa Geita
Una mpago gani na maendeleo ya Mkoa wa Geita maana tangu tumekuchagua hatujaona chochote?
Jibu: Mbunge ana mipango mizuri tu ya maendeleo ya
Geita na ndiyo maana mnaona sasa hivi Geita imebadilika haikuwa kama
ilivyokuwa mwanzo.
Tumejenga barabara za lami, tumefanya ukarabati wa baadhi ya
majengo ya Geita, bado tuna mipango mingi ya kuhakikisha Geita inakuwa
na maendeleo.
9. Simon Nyanda, mkazi wa Nyankumbu
Tangu tukupe madaraka hujawahi kutufanyia chochote
katika ahadi zote ulizotuahidi ikiwamo umeme katika Kijiji cha
Nyankumbu. Mpaka leo wananchi wanatumia vibatali. Zahanati ya Nyankumbu
kina mama wanajifungua kwa vibatali na tochi. Kwa muda huu uliobaki
utatufanyia nini?
Jibu: Kwa muda huu ulliobaki mbunge analifanyia
kazi suala hilo. Kuna mpango wa kusambaza umeme vijijini na vijiji 30
vya Jimbo la Geita vitanufaika kikiwamo Kijiji cha Nyankumbu na Zahanati
ya Nyankumbu.
Mchakato wa kusambaza umeme katika Jimbo la Geita
umeshaanza, nguzo zinasimikwa na kazi inafanyika kwa kasi hivyo muda si
mrefu umeme utawala Nyankumbu na Tarafa nzima ya Busanda.
10. Edward Kuzenza, mkazi wa Geita
Ulituhaidi kwamba hadi kufikia Novemba, 2011 wananchi wa Wilaya ya Geita watakuwa na maji.
Lakini mpaka sasa wanahangaika . Je, una mkakati gani wa kutuletea maji wakazi wa Geita?
Jibu: Nimeshaeleza kwamba maji yatafika Geita muda
ambao. Kama nilivyosema, bajeti ya mwaka huu ilibana kidogo kutokana na
mambo ya kitaifa.
Hivyo kufikia Novemba mwaka huu, wakazi wa Geita watakuwa na maji kama mbunge alivyoahidi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni