Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam, jana iliahirisha kutoa hukumu ya rufaa iliyofunguliwa na Katibu
wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda
hadi Novemba 27.
Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Augustine Shangwa aliiahirisha kesi hiyo kwa kuwa hukumu bado haijaandikwa.
Katika rufaa hiyo, Ponda anayetetewa na wakili
Juma Nassoro anapinga hatia ya adhabu aliyopewa katika hukumu ya
Mahakama ya Kisutu, akidai kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha kumtia
hatiani kwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.
Katika kesi ya msingi, Ponda na wenzake walikuwa
wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama, wizi wa mali yenye thamani ya
Sh59.6 milioni na kuingia kijinai kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali
eneo la ardhi inayomilikiwa na Kampuni ya Agritanza Ltd.
Ponda na mwenzake, Mukadamu Swaleh walikuwa wakikabiliwa na shtaka lingine la uchochezi.
Katika Mahakama ya Kisutu, hukumu ya Ponda
ilitolewa na Hakimu Mkazi Victoria Nongwa, Mei 9, 2013 na kumtia hatiani
kwa kosa la kuingia kijinai katika eneo hilo la ardhi, lakini
ikawaachia huru washtakiwa wengine.
Hata hivyo, licha ya kumtia hatiani Ponda,
Mahakama hiyo ilimwachia huru kwa masharti ya kutokutenda kosa lolote
katika kipindi cha mwaka mmoja, chini ya kifungu cha 25 (g) cha Sheria
ya Kanuni za Adhabu. Katika rufaa yake kupinga hukumu hiyo, Ponda
anadai kuwa Mahakama hiyo ilikosea kumtia hatiani kwa shtaka hilo kwa
kuwa hakukuwa na ushahidi wa kuingia kijinai katika eneo hilo.
Awali, kabla ya kuahirishwa, idadi kubwa ya
wafuasi wa Sheikh Ponda walifurika katika viwanja vya Mahakama ili kujua
hukumu itakayotolewa.
Nje ya mahakama hiyo, ulinzi mkali uliimarishwa
likiwamo gari moja la maji ya kuwasha, mbwa na askari waliokuwa na
silaha za moto na mabomu ya machozi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni